Imeelezwa kuwa Taifa litaokoa takribani Shilingi Bilioni 202 za
Kitanzania kwa mwaka endapo mradi wa usambazaji wa gesi asilia katika
jiji la Dar es Salaam utatekelezwa.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni mjini Dodoma katika Mkutano wa
Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste (CCT), wakati Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiwasilisha mada iliyohusu rasilimali
za mafuta na gesi kwa manufaa ya Watanzania wote.

Akielezea mradi husika, Waziri Muhongo alisema lengo kuu ni kuweka
mtandao wa mabomba ya kusambaza gesi na vituo vya kujazia gesi magari
ambapo ulifanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 2006/2007 na kuhusisha magari
8,000 na makazi yapatayo 30,000.

Profesa Muhongo alisema ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza Julai
2015 ambapo kwa sasa zoezi la kumtafuta Mkandarasi pamoja na fedha za
ujenzi takribani Dola za Marekani milioni 76 linaendelea.

 

Askofu
Dkt. Valentino Mokiwa wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam
akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo (hayupo pichani) baada ya Waziri huyo kuwasilisha mada katika
Mkutano wa Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste nchini (CCT).

Aidha, Waziri Muhongo alizungumzia faida iliyopatikana kitaifa kwa
kutumia gesi asilia kwa kipindi cha miaka 10 kutoka mwaka 2004 na
kubainisha kuwa Taifa limepata mapato kiasi cha Dola za Marekani 235.9
milioni.

Pia, alisema Taifa limeokoa kiasi cha Dola za Marekani 5.3 bilioni
katika kuzalisha umeme na kiasi cha Dola za Marekani 449.7 milioni
katika viwanda.

Manufaa mengine ni pamoja na Halmashauri husika hupata Kodi ya Huduma
(service levy) ambayo ni asilimia 0.3 ya mapato ya mauzo ya gesi.
Waziri Muhongo alitoa mfano wa mradi wa SongoSongo, ambapo Halmashauri
ya Kilwa hupata takribani shilingi za Tanzania milioni 100 kila baada ya
miezi mitatu.

Akizungumzia faida za bomba kuu la kusafisha na kusafirishia gesi
asilia ambalo ujenzi wake unaendelea, alisema mitambo iliyopo sasa,
imesababisha nchi kupoteza shilingi za Tanzania trilioni 1.6 kwa mwaka
kwa kutumia mafuta kuzalisha umeme badala ya gesi asilia.

Alisema endapo bomba hili litatumika katika kiwango chake cha juu
(784 mmscfd), gesi itakayosafirishwa kwa kipindi cha miaka 20 ni
asilimia 12 tu ya gesi iliyogunduliwa hadi sasa.

“Nchi itaokoa Dola za Marekani bilioni moja (sawa na shilingi za
Tanzania trilioni 1.6) kwa mwaka kutokana na mitambo iliyopo nchini
inayozalisha umeme kwa kutumia mafuta kuanza kutumia gesi asilia,”
alisema Waziri Muhongo.

Aidha, aliongeza kuwa bei ya uzalishaji umeme itapungua kwa uniti
moja (KWh) ambapo alifafanua kuwa umeme unaofuliwa kwa dizeli na mafuta
ya aina nyingine hugharimu senti za Marekani 30 hadi 45 wakati bei ya
kuzalisha uniti moja hiyo hiyo ni senti za Marekani saba kwa umeme
utokanao na gesi asilia.

Alizitaja faida nyingine za mradi mpya wa bomba la gesi kuwa ni
pamoja na ajira katika mitambo itakayojengwa Madimba na SongoSongo kwani
kila mtambo utahitaji kiasi cha wafanyakazi 60. Vilevile, alisema mradi
utatoa ajira katika sekta za afya, elimu, maji usafiri pamoja na huduma
nyingine za kijamii zitakazohitajika.
SOURCE;WWW.MEM.GO.TZ

Comment
50 replies

Comments are closed.