Kampuni ya Statoil Tanzania ina furaha kutangaza majina ya vijana watano waliongia fainali za shindano la biashara la mashujaa wa kesho ambalo lina dhumuni la kuhamasisha ujasiriamali kwa mikoa ya kusini mwa Tanzania yaani Mtwara na Lindi.
Akitoa taarifa hii meneja wa shindano hilo kutoka Statoil, Erick Mchome amewataja washindi hao kuwa ni Razaki Kaondo, Edward Timamu and Sifael Nkiliye (walioshiriki kama timu moja), Saleh Rashid Kisunga, Azizi Doa, na Yunus Mtopa.
Shindano la Mashujaa wa Kesho lilihusisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 25 kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi kuwasilisha mawazo yao ya biashara ambayo baadae yalibadilishwa na kuwekwa kwenye andiko la biashara.
Mwaka huu shindano hili lilivutia vijana zaidi ya 400 ambao waliwasilisha mawazo ya biashara zao zinazolenga sekta mbalimbali za uchumi kama kilimo, ufugaji, mawasiliano, na biashara nyingine ndogondogo. Vijana waliruhusiwa kushiriki mmoja mmoja au hata kuunda vikundi vya watu wawili mpaka watatu.